Registrar: registrar@judiciaryzanzibar.go.tz | Chief Court Administrator: cca@judiciaryzanzibar.go.tz

THE JUDICIARY ZANZIBAR

HOTUBA YA MHE JAJI MKUU WA ZANZIBAR KWENYE MKUTANO MKUU WA ZAJAO 2023

HOTUBA YA JAJI MKUU WA ZANZIBAR MHE. KHAMIS RAMADHAN ABDALLA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA ZAJOA WA MWAKA 2023

PAHALA: UKUMBI WA CHUO CHA UTALII MARUHUBI

TAREHE 06 APRILI, 2023.

MHESHIMIWA MWENYEKITI,

WAHESHMIWA MAJAJI WA MAHKAMA KUU MLIOPO,

MHESHMIWA KADHI MKUU WA ZANZIBAR,

MHESHMIWA NAIBU KADHI MKUU WA ZANZIBAR,

MHESHMIWA KADHI WA RUFAA PEMBA,

MHESHMIWA MTENDAJI MKUU WA MAHKAMA,

MHESHIWA MRAJIS WA MAHKAMA YA KADHI,

NAIBU WARAJIS WOTE MLIOPO,

WAHESHIMIWA WAJUMBE WOTE,

WAALIKWA NA WAFANYAKAZI WOTE WA MAHKAMA MLIOPO,

WAANDISHI WA HABARI,

MABIBI NA MABWANA,

ASALAM ALAYKUM ,

Ndugu Mwenyekiti,

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na utukufu kwa kutuvusha salama katika mwaka uliopita wa 2022 na kuingia mwaka mpya wa 2023 tukiwa tupo hai kwani baadhi yetu wameshatangulia akhera, Allah awape makaazi mema peponi Amin. Aidha, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema, salama, amani na utulivu katika nchi yetu na leo tumeweza kukutana hapa kwa ajili ya mkutano huu adhimu wa mwaka.


Ndugu Mwenyekiti na wajumbe,

Napenda kuchukua fursa hii, kuushukuru Uongozi wa ZAJOA kwa ujumla kwa kunialika tena kwa mara nyengine kuwa, Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huu wa mwaka na pia kuhudhuria mimi mwenyewe nikiwa ni mlezi wa ZAJOA na mjumbe wa mkutano huu. Hii ni fursa adhimu kwangu kwani huniwezesha kujumuika na waheshimiwa Majaji, Mahakimu na Makadhi na kupata wasaa wa kufahamu mafanikio na changamoto za ZAJOA na Mahkama kwa ujumla kwa mwaka uliopita pamoja na kufahamu malengo na mikakati kwa mwaka ujao ili kuboresha na kuimarisha utendaji kazi na utoaji haki nchini na hivyo, kuleta maendeleo ya Taifa kwa ujumla.


Ndugu Mwenyekiti,

Napenda kuipongeza ZAJOA kwa kuweza kuiwakilisha vizuri Mahkama Zanzibar na kushiriki kikamilifu katika mkutano wa EAMJA uliofanyika Kigali Rwanda mwaka jana ingawa mimi mwenyewe sikuweza kushiriki kutokana na majukumu mengine yaliyojitokeza lakini taarifa nilizopewa ni kuwa, mambo yamekwenda vizuri. Sambamba na hilo nawashukuru kwa dhati kabisa waheshimiwa Majaji, Mahakimu na Makadhi wote kwa kushiriki kikamilifu na kufanikisha maadhimisho ya siku ya sheria “LAW DAY“ ya mwaka huu.


Nyote mlikua ni mashahidi kwamba, sherehe zetu za siku ya sheria za mwaka huu zilikua na mambo mengi mapya na ya ubunifu mkubwa  kama vile mbio za marathon, uzinduzi wa ripoti ya mwaka ya utendaji kazi wa Mahkama, utoaji wa zawadi kwa vinara wa utoaji wa haki n.k, tujipongeze sote kwani sherehe zetu za siku ya sheria za mwaka huu zilifana sana kinyume na matarajio yetu.


Ndugu Mwenyekiti,

ZAJOA imeniarifu rasmi kwamba, mkutano wa Baraza kuu la Majaji na Mahakimu wa Afrika Mashariki (EAMJA COUNCIL MEETING) utafanyika hapa Zanzibar mnamo tarehe 23, juni 2023. Napenda kuwahakikishia kwamba, uongozi wa Mahkama kwa mashirikiano na ZAJOA utafanya kila kinachowezekana kuhakikisha kua, mkutano huo unafanyika kwa mafanikio makubwa na kuiletea sifa nchi yetu.


Ndugu Mwenyekiti,

Sasa nizungumzie utendaji kazi wetu wa Mahkama kwa mwaka uliopita.  Ripoti ya tathmini ya utendaji kazi wa Mahkama  inaonyesha kwamba, kwa ujumla, kwa mwaka 2022, Mahkama za Zanzibar zimeweza kumaliza mashauri ya jinai kwa asilimia 91.7% na kwa kesi za madai, kasi ya umalizikaji wa mashauri ni asilimia 54.9%. Takwimu hizo zinaonyesha kwamba,  hali ya umalizikaji wa mashauri ya jinai ni nzuri sana na kwa upande wa mashauri ya madai ni nzuri kiasi.

Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati , Waheshimiwa Majaji, Mahakimu, Warajis, Makadhi na Watumishi wote wa Mahkama kwa ari na moyo wa utendaji kazi tuliouonyesha kwa mwaka uliopita wa 2022. Mafanikio haya yasingepatikana kama sote tusingefanya kazi ya ziada.

Aidha pongezi ziwaendee wadau wetu wakuu ambao ni Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA), Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na madawa ya Kulevya, Chama cha Mawakili, Asasi za Kiraia na bila ya kuwasahau watu wenye mashauri (Wadaawa)

Ndugu Mwenyekiti,

Napenda nieleze kwamba, licha ya juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha utendaji kazi wa Mahkama, bado tunakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile uhaba wa watumishi uliosababishwa na watumishi wetu wengi kufikia umri wa kustaafu na wengine kufariki, uchakavu wa majengo na vitendea kazi n.k. Hata hivyo, niwahakikishie kua, kwa kushirikiana na Serikali yetu, tunaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi. Kwa mfano, katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa watumishi, kwa mwaka 2022/2023 serikali imeturuhusu kuajiri Makatibu muhtasi watano (5) na Maofisa Sheria watatu (3). Aidha, baada ya Serikali kupitisha muudo wa utawala wa Mahkama, tumepewa kibali cha kuajiri Mkurugenzi Mipango na Utafiti pamoja na Mkurugenzi Rasilimali watu na Utawala. Mchakato wa uajiri kwa watumishi wote hao upo kwenye hatua za mwisho na tunataraji hivi karibuni wataajiriwa. Kuajiriwa kwa watumishi hao kutasaidia sana kuongeza ufanisi katika shughuli zetu. Halkadhalika, katika mwaka mpya wa fedha wa 23/24, pia tutaendelea na zoezi la uajiri wa wafanyakazi wapya kwa lengo la kuziba mapengo ya watumishi (replacement) kwenye taasisi yetu.

Ndugu Mwenyekiti,

Hivi karibuni uongozi wa Mahkama uliamua kuwa, mfumo wa upandaji vyeo kwenye mhimili wetu uwe wa uwazi zaidi kwa nafasi husika kutangazwa na waombaji wakiwemo watumishi wetu wa Mahkama kuomba nafasi hizo na baadae kufanyiwa usaili. Tumeanzisha mfumo huu kwa nia njema kabisa ya kupata watendaji wenye sifa stahiki pamoja na kuondoa malalamiko yanayojitokeza kila tunapofanya mchakato wa upandishaji vyeo. Aidha, mfumo huu ni maarufu sana katika nchi za majirani zetu. Ombi langu kwenu ni kua, kwa wale watakaobahatika kupanda vyeo, waonyeshe kwa vitendo kuwa kweli walistahiki kupata nafasi hizo na wakati huo kwa wale ambao hawatobahatika kupata nafasi hizo, basi wasivunjike wala kukasirika bali nao wazidishe ari ya kufanya kazi huku wakijuwa kua, kuna fursa nyingi tu za wao kupanda madaraja muda si mrefu. Naipongeza sana Tume ya Utumishi wa Mahkama pamoja na Afisi ya Mtendaji Mkuu na ile ya Mrajis wa Mahkama kwa kusimamia kwa umakini zoezi hilo la ajira.

Ndugu Mwenyekiti,

Kama tulivyoeleza wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria ya mwaka huu kua,tumedhamiria kuelekea kwenye Mahkama Mtandao. Hivi sasa tupo kwenye hatua za mwisho zitakazotuwezesha kuingia kwenye uanzishaji wa mifumo mbali mbali ya kidijitali itakayorahisisha utendaji wetu wa kazi. Wakati hayo yakiendelea, natowa wito kwa watumishi wote wa Mahkama kujiendeleza katika fani ya teknolojia ya habari na matumizi ya Tehama ili wasije wakaachwa nyuma kwenye mabadiliko hayo ya kidigitali. Halkadhalika, Mahakama kwa kushirikiana na Serikali itaweka mazingira mazuri kwa ajili ya matumizi ya Tehama kama vile ujenzi wa majengo bora na ya kisasa ya Mahkama ili kuifanya azma hiyo ya mahakama mtandao iwe rahisi kutekelezeka.

Ndugu Mwenyekiti,

Serikali yetu inaelewa kuwa, mazingira mazuri ya utoaji haki ni lazima yaendane sambamba na uboreshaji wa maslahi ya watumishi wa sekta ya sheria. Hivyo, kuipitia mkutano huu napenda kuipongeza serikali yetu kwa kuongeza kwa kiasi kikubwa maslahi ya watumishi wa Mahkama pamoja na kumaliza kilio cha siku nyingi cha mishahara ya Mahakimu wa Mahkama za mwanzo. Aidha, Serikali imeridhia ombi letu la kuwalipa posho la mavazi (outfit allowance) watumishi wote wa Mahkama.


Nimefurahi sana baada ya Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahkama kuniarifu kuwa, zoezi la kuwalipa posho la mavazi  watumishi wote wa Mahkama limeanza na limeanzia kwa watumishi wa kada za chini kama vile matarishi, madereva, makarani n.k. Ni matumaini yangu kuwa, hatua hizo zitakuwa ni chachu ya kuongeza ari ya kufanya kazi kwa watumishi wetu.

Ndugu Mwenyekiti,

Nimefahamishwa kwamba, pamoja na mambo mengine, katika mkutano huu kutafanyika uchaguzi mkuu wa viongozi mbali mbali wa ZAJOA. Natowa wito kwa wajumbe, kuwachaguwa viongozi wenye sifa ambao watakuwa na uwezo mkubwa wa kutatua changamoto mbali mbali za ZAJOA ikiwemo ubunifu wa vyanzo mbali mbali vya mapato pamoja na kuiwalisha vizuri ZAJOA kwenye mikutano ya kimataifa. Halkadhalika, natowa wito kwa uongozi mpya wa ZAJOA utakaiongia madarakani baada ya uchaguzi kutengeneza mpango mkakati wa mafunzo kwa wanachama wake. Hii ni kwa sababu, fani ya sheria imekuwa inakuwa kwa kasi sana, hivyo wanachama wa ZAJOA wakiwemo Majaji, Mahakimu na Makadhi wanahitaji kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara kwa lengo la kukuza uelewa wao kwenye mambo mbali mbali yanayousu utendaji kazi wao.

Ndugu Mwenyekiti,

Nimefurahi sana baada ya kuambiwa kuwa mkutano huo utatanguliwa na uwasilishaji wa mada inayohusu njia za kudhibiti msongo wa mawazo (stress Management) pamoja na salamu za Benki ya NMB. Kwanza, nawapongeza na ninawashukuru watayarishaji wa mada zote zitakazowasilishwa hapa kwa uzalendo wao. Kwa upande wa mada ya kuondoa msongo wa mawazo, nasema kuwa ni mada muhimu sana kwa watendaji wa Mahkama hasa kwa vile itaimarisha afya ya akili zetu kutokana na kazi ngumu tulizonazo. Vile vile kwa upande wa Benki ya NMB nao nawashukuru na ninawaomba watuunge mkono katika shughuli zetu mbali mbali za kimahkama zitakazofuata.

Ndugu Mwenyekiti,

Kwa kumalizia,napenda  nitowe wito kwa ZAJOA kuwa, katika mkutano mkuu wa mwakani wa ZAJOA tutenge siku mbili ambapo siku ya kwanza iwe ni kwa ajili ya mafunzo na mambo mengine kama vile upimaji wa afya (medical checkup) n.k na siku ya pili iwe ni kwa ajili ya kufanya mkutano mkuu. Uongozi wa Mhkama upo tayari kuiwezesha ZAJOA kutatuwa changamoto mbali mbali inazozikabili kila hali itakaporuhusu. Mwisho kabisa nawaomba wajumbe wote kutumia mkutano huu kujadili changamoto mbali mbali zinazoikabili Mahkama na ZAJOA kwa njia za kistaarabu bila ya kumkwaza mtu na kupendekeza ufumbuzi wake. Nawatakia mkutano mwema na sasa natangaza rasmi kua,

MKUTANO HUU MKUU WA ZAJOA WA MWAKA 2023 UMEFUNGULIWA RASMI. AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA.

Unguja

High Court, Vuga
ZANZIBAR
Tel: +255 719 606 436
Email: info@judiciaryzanzibar.go.tz
Monday - Friday: 07:30am - 09:30pm
Saturday & Sunday: Closed

Pemba

High Court, Chake-Chake
ZANZIBAR
Tel: +255 719 606 436
Email: infopemba@judiciaryzanzibar.go.tz
Monday - Friday: 07:30am - 09:30pm
Saturday & Sunday: Closed