JAJI MKUU WA ZANZIBAR APOKEA RIPOTI YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA KAMATI YA NIDHAMU NA MAADILI KWA MAWAKILI NA MAVAKILI
2026-11-05
Zanzibar Judiciary
Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla amewataka mawakili kuhakikisha wanawapa wateja wao mrejesho wa mara kwa mara kuhusu maendeleo ya kesi wanazowawakilisha, akisisitiza kuwa mawasiliano kati ya wakili na mteja ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa majukumu ya taaluma ya uwakili.rnJaji Mkuu ameyasema hayo wakati akiongoza kikao cha upokeaji wa ripoti ya utendaji kazi ya Kamati ya Nidhamu ya Maadili ya Mawakili Zanzibar kwa kipindi cha mwaka 2024 hadi Agosti 2026, kilichofanyika tarehe 05 Novemba, 2026 Tunguu, Zanzibar. Akisisitiza kwamba kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuhusu mawakili kutopokea simu wala kujibu barua pepe (email) za wateja wao wanapotaka kufuatilia maendeleo ya kesi zao, hali inayoweza kusababisha wateja kukosa taarifa muhimu kuhusu mwenendo wa mashauri yao.rnAidha Mhe. Jaji Mkuu amekitaka Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS) kulichukulia suala la maadili ya mawakili kwa uzito unaostahiki na kuhakikisha kuwa wanachama wake wanazingatia misingi ya taaluma, uwajibikaji na mawasiliano mazuri na wateja wanaowahudumia.rnKwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2024 hadi 2026, Kamati imepokea jumla ya malalamiko 36 yaliyotolewa na wananchi dhidi ya Mawakili, ambapo malalamiko 33 yalifunguliwa rasmi na matatu yalifungwa bila kufunguliwa rasmi na malalamiko mengi yanahusu fedha zinazopokelewa na Mawakili kutoka kwa wateja kwa ajili ya kutekeleza huduma za kisheria lakini kushindwa kutoa huduma hizo kama zilivyokubaliwa.rnAmesema kuwa kutokana na malalamiko hayo, Kamati imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kinidhamu kulingana na uzito wa makosa yaliyothibitika, zikiwemo kufungia Mawakili kufanya kazi za uwakilishi kwa vipindi tofauti, kuwaagiza kurejesha fedha walizopokea kutoka kwa wateja bila kutekeleza huduma walizoahidi na kutoa onyo kwa makosa yanayobainika kuwa na uzito mdogo.rnAkizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti aliishukuru Mahkama kwa ushirikiano na imani iliyotolewa kwa Kamati, akisisitiza dhamira ya kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na kuzingatia misingi ya haki.rnNae, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) Ndugu Mgeni Jailani Jecha amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila wakili kuilinda na kuisimamia sheria inayodhibiti taaluma ya uwakili na Uvakili, badala ya kuwa sehemu ya vitendo vinavyoikiuka. Aidha, amewataka mawakili kuzingatia na kulinda maadili ya taaluma yao ili kudumisha heshima, uadilifu na imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji haki.rnAmeeleza kuwa uzingatiaji wa sheria na maadili ya kazi ni msingi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisheria zinazostahili na kuimarisha imani yao kwa taasisi za utoaji haki. Akifafanua kuwa wito huo unalenga kuimarisha uwajibikaji wa mawakili, kuboresha mahusiano kati yao na wateja pamoja na kuhakikisha taaluma ya uwakili inaendelea kusimama katika misingi ya weledi, uadilifu na heshima kwa sheria.