Skip to main content

New e-CMS system launching July 1, 2026 | Learn more

WATENDAJI WA MAHKAMA YA ZANZIBAR WAPATIWA MAFUNZO YA UANDAAJI WA BAJETI INAYOZINGATIA JINSIA

2026-10-29 Zanzibar Judiciary
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Zanzibar, Bi. Siti Abbas Ali, amewataka watendaji wa Mahkama ya Zanzibar kuhakikisha wanazingatia masuala ya jinsia katika uandaaji wa bajeti, mipango na utekelezaji wa shughuli mbalimbali, ili kuimarisha utoaji wa huduma zinazozingatia usawa na mahitaji ya makundi yote katika jamii.\r\nBi. Siti ameyasema hayo leo, tarehe 29 Oktoba, 2026, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wakuu wa Vittengo vya Mahkama kuhusu uandaaji wa bajeti inayozingatia jinsia, yanayofanyika katika Ofisi za ZAWA, Mwembe Madema, \r\nAmesema kuwa uandaaji wa bajeti inayozingatia jinsia ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinapangwa na kutumika kwa kuzingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya wananchi, hivyo kuwezesha kila mwananchi kunufaika na huduma zinazotolewa bila ubaguzi.\r\nAidha, amefafanua kuwa dhana ya bajeti inayozingatia jinsia haipaswi kujikita katika mahitaji ya wanawake na wanaume pekee, bali inapaswa kuzingatia pia mahitaji ya watu wenye ulemavu, wazee, watoto na makundi mengine yenye mahitaji maalumu katika jamii.\r\nAmesisitiza kuwa masuala ya jinsia yanapaswa kupewa kipaumbele katika upangaji na utoaji wa huduma muhimu za kijamii, zikiwemo elimu, afya, maji na huduma za haki, ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa urahisi na kwa kuzingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya wananchi.\r\nKatika hatua nyingine, Bi. Siti ameuomba uongozi wa Mahkama ya Zanzibar kuzingatia uwezekano wa kuweka angalau Afisa Jinsia mmoja katika kila jengo la Mahkama, kwa lengo la kuratibu na kusimamia masuala ya jinsia pamoja na kuhakikisha huduma za Mahkama zinatolewa kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wote.\r\nSambamba na hilo, ameipongeza Mahkama ya Zanzibar kwa juhudi inazoendelea kuzichukua katika kuboresha mazingira na huduma zinazozingatia masuala ya jinsia, akieleza kuwa hatua hizo zina mchango mkubwa katika kuimarisha usawa na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.\r\nVilevile, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia kikamilifu fursa waliyoipata kwa kujifunza na kuyafanyia kazi maarifa watakayoyapata, ili yaweze kuleta mabadiliko chanya katika uandaaji wa mipango, bajeti na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.\r\nAmeongeza kuwa ni muhimu kwa Mahkama ya Zanzibar kuendelea kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu masuala ya jinsia na bajeti inayozingatia jinsia, ili kuongeza uelewa wa watendaji na kuimarisha uwezo wa taasisi katika kutoa huduma bora, jumuishi na zenye usawa kwa wananchi.\r\nMafunzo hayo yanafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kupitia Mradi wa Maboresho ya Mahkama ya Zanzibar (Zi-JUMP), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezo wa watendaji wa Mahkama katika kuzingatia masuala ya jinsia kwenye mipango na bajeti za taasisi.\r\nMafunzo hayo yanaendeshwa na Dkt. Amon Katunzi, Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia na Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Kigamboni.