ZANZIBAR KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MAJAJI WAKUU WA NCHI ZA KUSINI NA MASHARIKI MWA AFRIKA – OKTOBA 2026
2026-08-20
Zanzibar Judiciary
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, amesema Zanzibar inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF), utakaofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 9 Oktoba 2026, katika Hoteli ya Verde, Mtoni, Zanzibar.\r\nJaji Mkuu ameyasema hayo leo, tarehe 20 Agosti 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mahkama Kuu Tunguu, kwa lengo la kuelezea maandalizi, umuhimu na manufaa ya mkutano huo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.\r\nAmesema Mahkama ya Zanzibar imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa, unaolenga kuwakutanisha Majaji Wakuu na viongozi wa Mahkama kutoka nchi 17 za Afrika kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazohusu utoaji wa haki na kuweka mikakati ya kuimarisha utawala wa sheria.\r\nMkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na takribani washiriki na waalikwa 150 kutoka Afrika na maeneo mengine duniani, wakiwemo Majaji Wakuu 16 kutoka nchi wanachama wa SEACJF.\r\nJaji Mkuu ameeleza kuwa miongoni mwa mada muhimu zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni uongozi wa Mahkama katika kusukuma mageuzi ya kitaasisi, njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR), mabadiliko ya kidijitali katika Mahkama, uimarishaji wa usimamizi wa Mahkama, pamoja na matumizi ya Akili Unde (AI) katika utoaji wa haki.\r\nAmeongeza kuwa mada inayohusu mabadiliko ya kidijitali katika Mahkama, ikijumuisha ufunguaji wa mashauri kwa njia ya kielektroniki, usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na mifumo ya usimamizi wa mashauri, itawasilishwa na wenyeji, Mahkama ya Zanzibar.\r\nAkizungumzia manufaa ya mkutano huo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Jaji Mkuu amesema mkutano huo utatoa fursa ya kuongeza ujuzi na kubadilishana uzoefu katika matumizi ya teknolojia katika Mahkama, Akili Unde, usimamizi wa mashauri na njia mbadala za utatuzi wa migogoro.\r\nAidha, mkutano huo unatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa baina ya Mahkama, kuitangaza Zanzibar kupitia utalii wa mikutano, kuchangia katika ongezeko la shughuli za kiuchumi na mapato ya Serikali, pamoja na kutoa fursa za mafunzo na kujenga uwezo wa Majaji na maofisa wa Mahkama.\r\nMkutano utafanyika chini ya kaulimbiu:\r\n“Transforming Justice Delivery: Innovation, Efficiency and Court Administration Reform.”\r\nKaulimbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa ubunifu, ufanisi na mageuzi katika usimamizi wa Mahkama ili kuimarisha utoaji wa haki.\r\nJaji Mkuu amesema miongoni mwa viongozi wakuu wanaotarajiwa kushiriki katika mkutano huo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi wa mkutano huo.\r\nPia, Makamu wa Rais wa Botswana na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Mhe. Ndaba Nkosinathi Gaolathe, anatarajiwa kuwa miongoni mwa viongozi watakaoshiriki katika mkutano huo.\r\nSEACJF ni jukwaa la kikanda lililoasisiwa mwaka 2003 nchini Afrika Kusini, linalowakutanisha viongozi wa mihimili ya utoaji haki kutoka takribani nchi 17 za Afrika. Jukwaa hilo linalenga kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma, kuboresha usimamizi wa Mahkama, kubadilishana uzoefu na kuendeleza misingi ya sheria na utawala bora. See less