JAJI MKUU WA ZANZIBAR AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA INDIA KUHUSU USHIRIKIANO WA MAENDELEO
2026-08-11
Zanzibar Judiciary
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, leo tarehe 11 Agosti 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Bishwadip Dey, katika Ofisi ya Jaji Mkuu, Mahkama Kuu Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.\r\nKatika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Mahkama ya Zanzibar na India, hususan katika maeneo ya maendeleo ya rasilimali watu na kubadilishana uzoefu na maarifa.\r\nMiongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni fursa za kuwaongezea uwezo na ujuzi watumishi wa Mahkama kupitia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu, pamoja na ziara za kimafunzo nchini India. Hatua hiyo inalenga kuwawezesha watumishi kupata maarifa na uzoefu utakaosaidia kuimarisha utendaji na utoaji wa huduma za haki.\r\nAidha, Mahkama ya Zanzibar inatarajia kuingia katika Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding – MoU) na upande wa India, ambayo itaweka msingi na maeneo mahsusi ya ushirikiano wenye manufaa kwa Mahkama ya Zanzibar na sekta ya haki kwa ujumla.\r\nUshirikiano huo unatarajiwa kuchangia katika kuimarisha uwezo wa Mahkama, kubadilishana uzoefu na maarifa, kujenga uwezo wa watumishi, pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.