MAKAMO WA PILI WA RAIS AIPONGEZA MAHKAMA YA ZANZIBAR KWA MAGEUZI YA UTOAJI HAKI KUPITIA TEHAMA
2026-02-09
Zanzibar Judiciary
MAKAMO WA PILI WA RAIS AIPONGEZA MAHKAMA YA ZANZIBAR KWA MAGEUZI YA UTOAJI HAKI KUPITIA TEHAMA\r\nMakamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema kuwa kauli mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Zanzibar 2026 inaakisi dhamira ya dhati ya Mahkama ya Zanzibar katika kuboresha utendaji wake pamoja na kuonesha maono mapana ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utoaji wa haki.\r\nAkizungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kilichofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete–Pemba, Mhe. Hemed amesema utekelezaji wa majukumu ya Mahkama unaendana kikamilifu na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, hususan katika ujenzi wa taasisi imara za haki na utawala bora.\r\nMakamo wa Pili wa Rais ameeleza kuwa Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 13.6 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Mahkama ya Zanzibar, hatua aliyosema inalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa Mahkama pamoja na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.\r\nAidha, ameeleza kufarajishwa kwake kwa kuona sheria mbalimbali zimepitiwa na kufanyiwa marekebisho ili ziendane na mazingira ya sasa pamoja na utungaji wa kanuni mpya zinazolenga kuongeza ufanisi na kasi ya utoaji wa haki. Aliinasihi Mahkama kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na uwajibikaji ili kufikia malengo yake na kutimiza azma ya wananchi juu ya Mahkama.\r\nMhe. Hemed amesema anaamini kuwa maboresho yaliyofanyika ndani ya Mahkama yatakuwa chachu ya maendeleo zaidi kwa mwaka 2026 na miaka inayofuata. Vilevile, alivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa mashirikiano makubwa wanayoyatoa kwa MhimiIi wa Mahkama na mihimili mingine ya Serikali katika kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa.\r\nKatika hatua nyingine, Makamo wa Pili wa Rais alitoa pongezi zake adhimu kwa Mahkama ya Zanzibar kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria 2026, pamoja na kuwashukuru watumishi mbalimbali kutoka Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju, kwa kushiriki katika kufanikisha maadhimisho hayo. \r\nAidha, ameipongeza Mahkama ya Zanzibar kwa kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii katika Wiki ya Sheria ikiwemo usafi wa mazingira na utoaji wa misaada kwa watu wa makundi maalum, kwani jambo hilo hujenga undugu kwa kuiweka jamii karibu na Mahkama na kuleta faraja kwa jamii.\r\nNae kwa upande wake Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla amesema kuwa Mahkama ya Zanzibar imechukua hatua mbalimbali za kimkakati katika kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA ikiwemo kukamilisha Mfumo wa ambao utarahisisha ufunguaji wa mashauri, ufuatiliaji wa mwenendo wa kesi na kupunguza matumizi ya karatasi. \r\nAmeeleza kuwa matumizi ya (TEHAMA) ni nyenzo muhimu inayoakisi mageuzi makubwa yanayoendelea ndani ya Mahkama pamoja na dira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuelekea katika mfumo wa Serikali Mtandao kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi, kupunguza ucheleweshaji wa mashauri na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za kimahkama \r\nMhe. Jaji Mkuu pia alieleza kuwa Mahkama imetunga kanuni mbalimbali mpya kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji wa haki, ikiwemo Kanuni za Madai madogo (Small Claims Rules), Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi (Election Petition Rules), Kanuni za Ada za Mahkama, Kanuni za Madalali wa Mahkama, Kanuni za Ndoa, Talaka na yanayohusiana nayo, Kanuni za Mwenendo wa Mahkama Kuu (Rufaa Kutoka Mahkama ya Kadhi wa Rufaa), Kanuni za Ushahidi wa Kielektroniki na Kanuni za Usikilizaji wa Mashauri ya Masafa (Remote Hearing Rules).\r\n\r\nAidha, amefahamisha kuwa katika Taarifa ya Utendaji Kazi wa Mahkama kwa mwaka 2025, jumla ya mashauri 10,938 yaliendeshwa katika Mahkama za Unguja na Pemba, ambapo mashauri 8,108 sawa na asilimia 74 yaliamuliwa. Aidha, Mahkama imefanikiwa kupunguza mrundikano wa mashauri ya zamani kutoka asilimia 47 hadi asilimia 18.\r\nKwa upande wa miundombinu, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuiwezesha Mahkama kifedha hali iliyopelekea kukamilika kwa ujenzi wa majengo manne ya Mahkama kati ya saba yaliyopangwa kwa mwaka 2025.\r\nAkihitimisha hotuba yake, Jaji Mkuu alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuiwezesha Mahkama, pamoja na kuishukuru Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo kwa mchango wao katika utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Mahkama (Zi-JUMP).\r\n\r\nAwali akitoa neno la shukrani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman, alimshukuru Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar.\r\nMhe. Haroun Ali Suleiman aliipongeza Mahkama ya Zanzibar kwa juhudi kubwa inazochukua katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki, hususan kupitia matumizi ya TEHAMA, maboresho ya sheria na kanuni pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya Mahkama. Alisema Wizara yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na MhimiIi wa Mahkama katika kusimamia na kuimarisha misingi ya katiba, sheria, utawala bora na haki kwa wananchi wote wa Zanzibar.\r\nMaadhimisho ya Wiki ya Sheria Zanzibar 2026 yamefanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Matumizi ya TEHAMA ni Chachu ya Upatikanaji wa Haki”, yakilenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kuimarisha ufanisi na uwazi wa utoaji haki nchini.