MAKAMO WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AWAHIMIZA WANANCHI KUFANYA MAZOEZI ILI KUJIKINGA NA MARADHI YASIYOAMBUKIZA
2026-02-08
Zanzibar Judiciary
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amewahimiza wadau wa sekta ya sheria nchini kukumbatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia kwani hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha mifumo ya utoaji haki na kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kwa ufanisi na wakati.\r\n\r\nMhe. Hemed ameyasema hayo baada ya matembezi ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyoanzia Chakechake hadi Gombani ya Kale Pemba akisistiza kuwa matembezi hayo hayakuwa tu sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Sheria bali pia yana mchango mkubwa katika kujenga afya kwa washiriki na kuimarisha mwili.\r\n\r\nAidha, amefahamisha kuwa mabadiliko yanayotokea katika sekta ya utoaji haki ikiwemo matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika usajili, malipo, uendeshaji na usikilizaji wa mashauri, yanakwenda sambamba na juhudi za Serikali katika ujenzi na uimarishaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo Barabara, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo kote nchini ikiwemo ujenzi wa Uwanja mpya wa AFCON unaojengwa Fumba-Unguja unaotarajiwa kutumika katika mashindano ya AFCON 2027, \r\n\r\nVilevile, amewapongeza viongozi wa Serikali walioshiriki matembezi hayo pamoja na Kamati ya Maandalizi kwa kazi nzuri na usimamizi mzuri wa tukio hilo, na amemalizia kwa kutoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kuendeleza mazoezi ya mwili kwa kufanya angalau dakika 30 kwa siku, badala ya kusubiri siku maalum za matembezi, sambamba kuwanasihi kuzingatia ulaji bora na mpangilio mzuri wa chakula ili kujiepusha na maradhi yasiyoambukiza.\r\nMhe. Hemed ametoa shukrani zake za dhati kwa Jaji Mkuu wa Zanzibar kwa kumualika kuwa mgeni rasmi wa matembezi hayo, na kuipongeza Mahkama ya Zanzibar kwa kuendelea kuandaa shughuli zinazohamasisha ushiriki wa wananchi, na kuwataka wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa aujumla kuendelea kuilinda amani ya nchi, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya Zanzibar, Tanzania na dunia kwa ujumla.\r\n\r\nKwa upande wake Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, amewashukuru wananchi wote walioshiriki matembezi ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, vikiwemo vikundi mbalimbali vya wanamichezo kutoka Kisiwani Pemba, kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha mshikamano katika kuadhimisha tukio hilo muhimu.\r\n\r\nAidha Mhe. Jaji Mkuu amewaomba wananchi kushiriki kikamilifu katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria litakalofanyika tarehe 9 Februari 2026, Wete-Pemba saa mbili kamili za asubuhi. \r\n\r\nKilele hicho kinatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Hussein Ali Mwinyi, ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.