Skip to main content

New e-CMS system launching February 1, 2026 | Learn more

MAHAKAMA YA ZANZIBAR YAWEKA MSISITIZO MKAKATI WA USAWA WA KIJINSIA.

2026-01-22 Zanzibar Judiciary
MAHAKAMA YA ZANZIBAR YAWEKA MSISITIZO MKAKATI WA USAWA WA KIJINSIA.\r\nJaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla amesema kuwa Mahkama ya Zanzibar inaendelea kuimarisha jitihada za kukuza usawa wa kijinsia ndani ya mfumo wa utoaji haki, ikiwa ni sehemu ya mageuzi ya kiutendaji yanayolenga kuhakikisha haki inapatikana kwa usawa kwa wanawake, wanaume na makundi maalum katika jamii.\r\nAkizungumza wakati akifungua mafunzo ya Mkakati wa Haki za Kijinsia (2026-2030) katika hoteli ya Madinat Al Bahr Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi, amesema kuwa mkakati huo ni nyenzo muhimu katika kujenga mfumo wa haki unaozingatia misingi ya usawa na jumuishi. \r\nAlibainisha kuwa Mahkama inatambua changamoto za kijinsia zilizopo katika jamii na namna zinavyoathiri upatikanaji wa haki kwa baadhi ya makundi, hususan wanawake na Watoto, hivyo ni dhamira ya Mahkama kujenga taasisi jumuishi, yenye uwajibikaji na inayozingatia misingi ya haki na usawa kwa wote.\r\nJaji Mkuu ameeleza kuwa Mkakati wa Haki za Kijinsia umeandaliwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi ndani ya Mahkama, kuongeza ushiriki wa kijinsia katika nafasi za uongozi, pamoja na kuhakikisha huduma za kimahkama zinatolewa kwa kuzingatia mahitaji ya jinsia zote bila ubaguzi.\r\nAidha, alisisitiza kuwa utekelezaji wa mkakati huo utahusisha mafunzo kwa watumishi wa Mahkama, maboresho ya sera na taratibu, pamoja na ushirikiano na wadau mbalimbali wa haki nchini ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa. \r\nAidha Mhe Jaji Mkuu, alieleza kuwa Mahkama itaendelea kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mkakati wa jinsia ili kuhakikisha unaleta matokeo chanya katika utoaji haki na kuimarisha imani ya wananchi kwa mhimili wa Mahkama.\r\nNae, Mratibu wa Mradi wa Maboresho ya Mahkama (Zi-JUMP), Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, amesema kuwa Mahkama imeanza utekelezaji wa mafunzo ya awali ya Mkakati wa Haki za Kijinsia kwa wakuu wa taasisi zinazosimamia haki, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia katika utoaji wa haki, amabapo mafunzo hayo yatafanyika katika awamu tatu tofauti ikiwemo; wakuu wa taasisi, mahakimu na makadhi na wafanyakazi wa kawaida wa mahkama \r\nJaji Ibrahim ameongeza kuwa mafunzo hayo yamekuwa fursa muhimu kwa washiriki kutoa maoni na michango yao kuhusu mkakati uliowasilishwa, kwa lengo la kuboresha zaidi kabla ya kuanza kutumika rasmi na hatimae kupata mkakati wenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.\r\nKwa upande wake, muwezeshaji wa mafunzo ya Mkakati wa Haki za Kijinsia Nd. Carsten Mahnke kutoka Ujerumani ameushukuru uongozi wa Mahkama kwa kumualika na kumpa nafasi ya kuwasilisha mafunzo ya mkakati huo, pamoja na kuwashukuru wadau wote wakiwemo taasisi za Serikali, taasisi binafsi na wananchi kwa ujumla ambao wamesaidia katika ukusanyaji na upatikanaji wa taarifa zilizotumika kuandaa mkakati huo unaolenga kuwa katika viwango vya kimataifa.\r\nAmeeleza kuwa lengo kuu la warsha hiyo ni kubadilishana mawazo, uzoefu na kutoa mapendekezo mbalimbali yatakayosaidia kutengeneza mkakati bora, jumuishi na unaoendana na mahitaji halisi ya taasisi za haki na jamii kwa ujumla.