WASHIRIKI WA MAFUNZO YA USAWA WA KIJINSIA WATAKIWA KUTUMIA MAFUNZO KUBORESHA HUDUMA ZA KIMAHKAMA
2026-01-22
Zanzibar Judiciary
Washiriki wa mafunzo ya usawa wa kijinsia wametakiwa kuyatumia ipasavyo mafunzo waliyopewa ili kuboresha utendaji wao wa kazi na kuimarisha utoaji wa huduma za kimahkama kwa ufanisi zaidi.\r\n\r\nAkizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya usawa wa kijinsia yaliyofanyika Madinatul-Bahar, Mbweni , kwa watendaji mbalimbali wa Mahkama pamoja na wadau ya Mahkama, Jaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar Mhe. Ibrahimu Mzee Ibrahim amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuboresha utoaji wa haki kwa kuzingatia misingi ya usawa wa kijinsia kwa watendaji na jamii kwa ujumla.\r\n\r\nMhe. Ibrahimu amewasisitiza washiriki kutumia muongozo waliopatiwa kama nyenzo muhimu ya kuboresha utendaji wa Mahkama na kusaidia jamii kupata haki kwa usawa. Ameeleza kuwa kuwajengea uwezo watendaji mbalimbali ni hatua muhimu katika kuimarisha utoaji wa huduma bora, za haki na zenye ufanisi.\r\n\r\nAidha, amebainisha kuwa kila mfanyakazi ana nafasi muhimu katika mnyororo wa utoaji wa huduma za kimahkama, hivyo ni lazima kila mmoja apatiwe mafunzo stahiki ili kuhakikisha malengo ya usawa wa kijinsia yanatekelezwa kikamilifu kwa wanajamii wanaohitaji haki.\r\n\r\nKwa upande wao, wakufunzi wa mafunzo hayo, Dr. Karen Muller na Karen Hollely kutoka Taasisi ya Ushahidi wa Watoto (Child Witness Institute) ya Afrika Kusini, wamesema kuwa haki na usawa katika jamii vitaweza kupatikana iwapo kila mtendaji atatekeleza majukumu yake kwa uwajibikaji na kuzingatia misingi ya usawa wa kijinsia.\r\n\r\nNao washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa wamepata uelewa mpana na watahakikisha wanabadilisha mtazamo wa wananchi kwa kuimarisha upatikanaji wa haki kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika maeneo yao ya kazi.\r\n\r\nMafunzo hayo ya siku nane yameendesha na Mahkama ya Zanzibar kupitia na Mradi wa Maboresho ya Mahkama ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mifumo ya utoaji wa haki na kulinda haki za makundi yote katika jamii.