Skip to main content

New e-CMS system launching February 1, 2026 | Learn more

JAJI AZIZA AONGEA NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU KONGAMANO LA SIKU 16 ZA KUPINGA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA

2025-12-01 Zanzibar Judiciary
Makamo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa upande wa Zanzibar Mhe. Jaji Aziza Iddi Suwedi, ameitaka jamii kupinga ukatili wa kijinsia na kuhakikisha kua jamii inalinda haki, usalama na utu wa wanawake, watoto na makundi yote yaliyo katika hatari ya kukumbwa na ukatili huo. \r\n\r\nJaji Aziza ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari huko Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambapo alitoa ufafanuzi juu ya kampeni ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia, huku akisisitiza kua ukatili wa kijinsia ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na TAWJA inaungana na taasisi zote za kisheria na kijamii kuhakikisha inatoa elimu kwa lengo la kuwalinda wahanga na kuharakisha upatikanaji wa haki. \r\n\r\nJaji Aziza amefafanua kuwa katika kipindi cha Siku 16, TAWJA itajikita katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na haki za wahanga, pamoja na kuhamasisha wananchi kuripoti matukio ya ukatili bila woga. Aidha, kampeni hii itahusisha ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali wakiwemo polisi, waendesha Mashtaka, viongozi wa dini, Taasisi za Elimu na jamii kwa ujumla, ili kutoa elimu na kuhakikisha mchakato wa utoaji haki unasimamiwa ipasavyo. \r\n\r\nJaji Aziza pia ametoa wito kwa wanaume kutoona aibu kujitokeza mahakamani na kufungua kesi za ukatili wa kijinsia pindi wanapofanyiwa hivyo na wenza wao au katika mazingira yoyote ya kijamii kwani ukatili wa kijinsia haupo tu kwa jinsia ya kike pekee na watoto badala yake huwakumba hata upande wa jinsia ya kiume. \r\n\r\nAidha, amemshukuru Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla na uongozi wa Mahkama ya Zanzibar kwa ujumla kwa ushirikiano wao wanaoutoa kwa taasisi ya TAWJA kwa lengo la kusimamia na kuharakisha utolewaji wa hukumu kwa kesi za ukatili wa kijinsia kwani jambo hilo linajenga matumaini na imani kubwa kwa Mahkama kutoka kwa wahanga.\r\n \r\nAmemalizia kwa kuishajihisha jamii kujitokeza kwa wingi katika shughuli mbalimbali zilizopangwa kufanyika katika kuadhimisha siku 16 za kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia ikiwemo kongamano kubwa litakalofanyika tarehe 06/12/2025 ambapo mama Maryam Mwinyi anatarajiwa kua mgeni rasmi.