JAJI FATMA HAMID MAHMOUD AFUNGUA MAFUNZO YA UANDISHI WA HUKUMU
2025-10-20
Zanzibar Judiciary
JAJI FATMA HAMID MAHMOUD AFUNGUA MAFUNZO YA UANDISHI WA HUKUMU, \r\n\r\nJaji wa Mahakama ya Kuu Zanzibar, Mhe. Fatma Hamid Mahmoud amesema kuwa umahiri katika uandishi wa hukumu, uelewa wa kisheria katika usikilizwaji wa mashahidi, pamoja na uandaaji wa amri za mahkama na utekelezaji wake hukuza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa haki.\r\n\r\nMhe. Jaji Fatma ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla yanayohusu Uandishi wa Hukumu, Ushughulikaji wa Mashahidi, Uandaaji wa Amri za Mahakama pamoja na Utekelezaji wake yanayofanyika katika Hoteli ya Madinatul Bahri, Zanzibar.\r\n\r\nAmesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuboresha ufanisi kwa Majaji na Makadhi katika kuandika hukumu zenye ubora, pamoja na kuhakikisha kuwa mashauri yanatolewa maamuzi kwa wakati na kwa mujibu wa sheria zilizopo.\r\n\r\nKwa upande wake, Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar Mhe. Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, ambae pia ni mratibu wa kitengo cha Maboresho ya Mahkama ameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka, kwani yataleta mabadiliko chanya katika mwenendo wa utoaji wa haki Zanzibar. Amesisitiza kuwa mafunzo ya namna hii ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kimkakati wa Mahkama unaolenga kuboresha ufanisi na kupunguza ucheleweshaji wa kesi Mahkamani.\r\n\r\nNae Mkufunzi wa mafunzo hayo Jaji wa Mahkama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Prof. Ubenna John Agatho, amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kujenga uelewa wa kina kuhusu mbinu bora za uandishi wa hukumu na usikilizwaji wa mashahidi. Ameeleza kuwa suala la uandaaji wa amri za mahkama na utekelezaji wake linahitaji umakini mkubwa, ili kuhakikisha haki inatendeka kikamilifu.\r\n\r\nAmeongeza kuwa mafunzo hayo yamezingatia pia changamoto za kiutendaji zinazojitokeza wakati wa kusikiliza mashahidi, ikiwemo mashahidi wenye uhasama, wale walio hatarini, na mashahidi wenye ulemavu.\r\n\r\nKwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wamemshukuru uongozi wa Mahkama ya Zanzibar kwa kuandaa mafunzo hayo wakisema kuwa yatawajengea uwezo mkubwa katika nyanja za kiutendaji. Wamesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kuandika hukumu kwa ufasaha, kuendesha mashauri kwa haki, na kuhakikisha amri za ahakama zinatekelezwa ipasavyo.