JAJI KHADIJA SHAMTE MZEE AFUNGUA MAFUNZO YA UPOKEAJ KANUNI ZA USHAHIDI WA ELEKTRONIKI
2025-10-17
Zanzibar Judiciary
JAJI WA MAHKAMA KUU ZANZIBAR MHE. KADHIJA SHAMTE MZEE AFUNGUA MAFUNZO YA KANUNI ZA UPOKEAJI WA USHAHIDI WA ELEKTRONIKI KATIKA MAHKAMA\r\n\r\nJaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar, Mhe. Khadija Shamte Mzee amesema kuwa dunia ya sasa imeingia katika zama za matumizi ya teknolojia ambapo ushahidi mwingi wa kesi, hasa zile zinazohusiana na makosa ya mtandao, unawasilishwa kwa njia ya kielektroniki. Hivyo, ni muhimu kwa Mahakimu, Makadhi na wadau wanaohusika katika uendeshaji wa kesi Mahkamani kujua namna sahihi ya kupokea, kutathmini na kutumia ushahidi huo kwa mujibu wa sheria.\r\n\r\nMhe. Khadija, ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu kanuni za Upokeaji wa Ushahidi kwa Njia ya kielektroniki kwa Mahakimu, Makadhi na wadau wengine muhimu wa Mahkama, yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahkama ya Mkoa wa Mjini Magharibi iliyopo Mazizini Zanzibar.\r\nAidha, ameeleza kua mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji hao wa Mahkama katika kutumia mbinu za kisasa za kisheria na kiteknolojia katika usikilizaji na utoaji wa maamuzi ya mashauri yanayohusisha ushahidi wa kielektroniki.\r\n\r\nAmesema kua teknolojia imebadilisha mfumo wa upatikanaji wa ushahidi, ambapo ushahidi haupo tu katika nyaraka au mashahidi wa mdomo, bali upo pia katika simu, kompyuta na mitandao ya kijamii kwa ujumla. Hivyo, ni jukumu la watendaji wa Mahkama kuhakikisha wanautumia ushahidi wa aina hiyo kwa weledi na kwa mujibu wa kanuni za kisheria.\r\n\r\nAmesisitiza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuondoa changamoto zinazojitokeza wakati wa kusikiliza mashauri yanayohusisha ushahidi wa kielektroniki, sambamba na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki kwa haraka na kwa usahihi.\r\n\r\nKwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo aweishukuru Mahkama ya Zanzibar kwa kuona umuhimu wa kuwapatia elimu hiyo, akisema itawasaidia kuongeza uelewa katika matumizi ya ushahidi wa teknolojia ya kisasa.