Registrar: registrar@judiciaryzanzibar.go.tz | Chief Court Administrator: cca@judiciaryzanzibar.go.tz

THE JUDICIARY OF ZANZIBAR

HOTUBA YA MHE. JAJI MKUU WA ZANZIBAR KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA

Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi;

Mhe. Prof Ibrahim Juma Hamisi: Jaji Mkuu wa Tanzania;

Mhe. Mustafa Mohammed Siyani Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania;

Waheshimiwa Majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar mliopo;

Waheshimiwa Mawaziri wote mliopo;

Mhe. Hassan Othman Ngwali Kadhi Mkuu Zanzibar;

Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar;

Mhe. Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar;

Mhe. Naibu Kadhi Mkuu Zanzibar;

Mhe. Mkuu wa Mkoa Kusini;

Mhe. Mrajis, Mahakama Kuu;

Mhe. Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania;

Mhe. Msajili Mahakama ya Rufani ya Tanzania;

Mtendaji Mkuu wa Mahakama Zanzibar;

Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Viongozi mbalimbali wa Serikali mliopo;

Viongozi wa Vyama mbalimbali vya Siasa mliopo;

Rais wa Jumuiya ya Wanasheria Zanzibar;

Mhe. Mrajisi Mahkama ya Kadhi;

Waheshmiwa Naibu Warajisi, Mahakimu, Makadhi na Wafanyakazi wote wa Mahkama pamoja na wadau wote wa Sheria mliopo;

Waandishi wa habari, Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana;

‘’ASALAAM ALEIKUM’’

--------------

MHESHIMIWA MGENI RASMI

Awali ya yote napenda niungane na wenzangu walionitangulia kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa neema ya uhai na uzima na kutuwezesha kukutana mahali hapa kwa ajili ya shughuli yetu hii adhimu  ya Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria Zanzibar.

Aidha, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Mgeni Rasmi kwa mara nyengine tena kukubali ombi letu la kuwa Mgeni Rasmi kwenye shughuli yetu hii, licha ya majukumu mengi ya kitaifa yanayokukabili.

Vilevile, napenda niwashukuru washiriki na waalikwa wote kutoka ndani na nje ya Zanzibar ukiwemo ujumbe wa Mahkama ya Tanzania ukiongozwa na mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma kwa kuacha shughuli zenu muhimu na kuungana nasi katika kufanikisha Sherehe zetu hizi za wiki na  Kilele cha siku ya Sheria. Nasema ahsante nyote na karibuni Zanzibar.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Maadhimisho haya ya Siku ya Sheria Zanzibar yalianza mwaka 2012, hivyo mwaka huu ni maadhimisho yetu ya kumi na mbili (12). Maadhimisho haya  vilevile yanafanyika Kisiwani Pemba na Mgeni Rasmi ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Kilele cha Siku ya Sheria hutanguliwa na shamrashamra za wiki ya Sheria ambapo mwaka huu zilianza rasmi tarehe 06 Febuari, 2023. Shughuli mbalimbali zilifanyika Unguja na Pemba zikiwemo Jaji Mkuu kuongea na waandishi wa Habari, utoaji wa  elimu kwa jamii katika maeneo mbalimbali ya miji vijiji na visiwa vidigo vidogo na Mashuleni.

Halikadhalika, elimu ilitolewa katika vyombo vya habari na makongamano. Shughuli nyengine iliyofanyika katika shamrashamra hizo ni wa kutambua mchango wa Mahakimu na Makadhi kwa kuwatunuku vyeti vinara wa utoaji wa Haki.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Kilele cha siku ya sheria, vilevile kilitanguliwa kwa kuwapokea Mawakili wapya kufanya kazi katika Mahkama zetu za Zanzibar pamoja na kuzindua mfumo wa kusajili Mawakili kwa kutumia Mtandao (Zan Wakili).

Shamrashamra hizo zilihitimishwa kwa matemebezi rasmi pamoja na mbio ndefu (law marathon) ya siku ya sharia yaliyobeba ujumbe wa kupiga vita udhalilishaji wa kijinsia ambayo yalitayarishwa kwa pamoja na Taasisi ya Zanzibar ya Maisha Bora Foundation. Mgeni rasmi wa Matembezi hayo alikuwa ni Mama Maryam Mwinyi-Mwenyekiti wa Taasisi hiyo.

MHEHIMIWA MGENI RASMI;

Matembezi hayo yalifana sana na wananchi wengi walishiriki na kupata ujumbe uliokusudiwa  wa kupinga vitendo vya udhalilishaji na haja ya kuwasaidia Wahanga wa makosa ya udhalilishaji wa Kijinsia.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Maadhimisho ya siku ya sheria yamekuwa yakiadhimishwa kwa kauli mbiu maalum. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘’HAKI MTANDAO KWA KUKUZA UCHUMI NA USTAWI WA JAMII’’.

Tumechagua Kaulimbiu hii kwa makusudi kwa vile suala la Haki Mtandao sio la Mahakama pekee bali ni la wadau wote wanaosimamia masuala ya Haki, kama vile Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, Jeshi la Polisi, Vyuo vya Mafunzo, Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, Asasi za kiraia na wadau wengine wanaohusika na masuala ya usimamizi na utoaji haki.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Ukuaji wa teknolojia ya Tehama duniani kwa kiasi kikubwa umerahisisha ukuaji wa uchumi katika nchi mbalimbali. Tunatambua juhudi za Serikali za kuanzisha mifumo mbalimbali ya Tehama ikiwemo: Afisi Mtandao (e-office), manunuzi mtandao (e-procurement) malipo mtandao (zan malipo) n.k. Mifumo hii inarahisisha utendaji kazi kwa haraka, huziba mianya ya upotevu wa fedha, kuondosha mianya ya rushwa, kufanya kazi kwa uwazi, kuongeza mapato pamoja na kuleta uwazi na ufanisi katika shughuli za kiutendaji wa Serikali.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Muhimili wa Mahkama unaunga mkono juhudi hizo kwa kuanzisha baadhi ya mifumo ya kielektroniki kama  vile mfumo wa usajili na usimamizi wa mawakili (ZanWakili) ambao ushaanza kutumika kwa mwaka huu 2023, Mfumo wa usimamizi wa mashauri kwa Mahkama Kuu na Mfumo wa uhifadhi wa hukumu za Mahkama Kuu (ZanLii) ambao kwa sasa Waheshimiwa Majaji hutuma Hukumu zao kwenye mfumo huo.

MHESHMIWA MGENI RASMI,

Matumizi ya Tehama katika Taasisi za Sheria yatawaondoshea wananchi usumbufu kwani wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali kama vile kufungua kesi, usikilizaji wa Mashauri, upokezi wa hukumu, upatikanaji wa Mienendo ya Kesi, mfumo wa kupokea malalamiko na utoaji wa maoni n.k.

Mifumo hii itaweza kupunguza muda ambapo shauri linakaa mahkamani, itafanya mashauri yamuuliwe kwa haraka na wananchi watapata muda wa kutosha wa kutumia katika shughuli za kujitafutia riziki na kukuza uchumi na vipato vyao.

Halikadhalika, kwa kuwepo uwazi katika usikilizaji wa Mashauri imani ya wananchi na Serikali kwa chombo cha Mahkama itapatikana.

MHESHMIWA MGENI RASMI,

Napenda kukujulisha kwamba, Mahkama kupitia Mradi wa Uimarishaji Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa taarifa za kesi kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Disemba 2022 ilipangiwa kutumia jumla ya shilingi  1,000,000,000/- (bilioni moja)kwa uanzishaji na uendelezaji mifumo mbalimbali lakini hadi sasa bado haijapatiwa fedha hizo kutoka Serikalini. Kwa heshima tunaomba kupatiwa fedha hizo ili kukamilisha mpango huo.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Sambamba na hilo, Kwa kuwa mifumo ya tehama hutegemea uwepo wa Majengo bora ya kisasa, Kwa mwaka 2022-2023 Mahkama kupitia mradi wa Ujenzi wa Mahkama za Mikoa kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2023 ilipangiwa kutumia jumla Shilingi 3,500,000,000/- (bilioni tatu na milioni mia tano) lakini hadi sasa hatujapata fedha hizo kutoka Serikalini.

Halikadhalika tunaiomba Serikali iidhinishe fedha hizo kwa matumizi hayo.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Napenda kutoa taarifa ya kuwa Mahkama kama ulivyotuagiza imeshatafuta  viwanja katika sehemu mbalimbali za Unguja na Pemba kwa madhumuni ya kujenga mahkama za Mikoa na Wilaya. Viwanja hivyo vimepatikana katika eneo la Kigunda Wilaya Kaskazini ‘’A’’ kwa madhumuni ya kujenga Mahkama ya Wilaya ili kusogeza huduma kwa Wananchi wa maeneo ya Kitalii Nungwi, Kendwa na Vitongoji vyake ambapo maeneo hayo idadi ya watu na shughuli za kijamii na kitalii zinakuwa kwa kasi.

Vilevile, Mahkama imeshapata Kiwanja eneo la Pale kwa madhumuni ya kujenga Mahkama ya Mkoa Kaskazini Unguja. Maeneo mengine ambayo Mahakama imepata Kiwanja ni eneo la Kinduni kwa madhumuni ya ujenzi wa Mahkama ya wilaya Kaskazini ‘’B’’, Kijichi kwa Wilaya ya Magharib ‘’A’’ na Mazizini kwa madhumuni ya kujenga Mahkama ya Mkoa Mjini Magharib.

Kwa upande wa Mkoa Kusini Unguja, Mahkama imepata eneo kwa ajili ya kujenga Mahkama ya Mkoa Kusini hapo Binguni na Makunduchi kwa Madhumuni ya kujenga Mahkama ya Wilaya Kusini.

Kwa upande wa Pemba, Mahkama imepata kiwanja Chakechake kwa madhumuni ya kujenga Mahkama Kuu katika eneo la Mabaoni. Changaweni Mkoani kwa ajili ya kujenga mahkama ya wilaya ya Mkoani.

Kwa upande wa Kaskazini Pemba Mahkama imepata kiwanja katika eneo la Kinyasini kwa madhumuni ya kujenga Mahkama ya Mkoa Kaskazini Pemba na Konde kwa ajili ya kujenga Mahkama ya wilaya ya Micheweni.

Hatua zote za kutafuta hati za Viwanja hivyo zimeshafikishwa katika Wizara ya ardhi, dizaini na michoro tayari zimeshatayarishwa na thamani za vipando na mali kwa ajili ya kulipa fidia wananchi kwa ajili kupisha ujenzi huo zimeshatathminiwa na fedha za kuwalipa wananchi hao zipo.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Ujenzi wa majengo hayo kutaifanya Mahkama kuwa katika mazingira bora na rafiki kuingia katika matumizi ya Mahkama mtandao.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Naomba kwa kifupi nitoe maelezo ya utendaji wa mahkama kwa mwaka wa Mahkama 2022.

Maelezo ya kina yameelezwa vizuri katika Ripoti ambayo nitakukabidhi.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Jukumu la msingi la Mahkama ni kupokea, kusikiliza na kuyatolea maamuzi mashauri yote ya jinai na madai. Hivyo, Kwa mwaka 2022 Mahkama za Unguja  zilipokea jumla ya mashauri ya jinai 15,159 ambapo kati ya hayo mashauri 13,712  yalitolewa maamuzi sawa na asilimia 90.5%.

Kwa upande wa Mahkama za Pemba zilipokea jumla ya mashauri 2,725  ya jinai ambapo mashauri 2,410  yaliamuliwa na kutolewa maamuzi sawa na asilimia 88.4%.

Kwa upande wa kesi za madai Mahkama za Unguja zilipokea jumla ya mashauri ya madai 1,616  ambapo kati ya hapo 752 yalitolewa maamuzi sawa na asilimia 46.5%.

Kwa upande wa Pemba, Mahkama zilipokea jumla ya mashauri ya madai 622 ambapo kati ya hayo mashauri 303 yaliamuliwa na kutolewa maamuzi sawa na asilimia 48.7%.

Vile vile, Mahkama za udhalilishaji za Unguja zilipokea jumla ya mashauri 1043 ambapo kati ya hayo mashauri 702 yaliamuliwa na kutolewa maamuzi sawa na asilimia 67.3%.

Kwa upande wa Pemba Mahkama za Udhalilishaji zilipokea jumla ya mashauri 238 ambapo kati ya hayo mashauri 173 yaliamuliwa na kutolewa maamuzi sawa na asilimia 72.7%.

Kwa upande wa Mahkama maalum za Makosa ya Madawa ya Kulevya za Unguja zilipokea jumla ya mashauri 543 ambapo kati ya hayo jumla ya mashauri 278 yaliamuliwa sawa na asilimia 51.2%.

Kwa upande Pemba Mahkama za Makosa ya Madawa ya Kulevya zilipokea jumla ya mashauri 83 ambapo kati ya hayo jumla ya mashauri 48 yalitolewa uamuzi sawa na asilimia 57.8%.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Mahkama za Kadhi nazo kwa upande wa Unguja zilipokea jumla ya mashauri 2,179  ambapo kati ya  hayo jumla ya mashauri 1,508  yaliamuliwa na kutolewa maamuzi sawa na asilimia 69.2%.

Mahkama za Kadhi za Pemba nazo zilipokea jumla ya mashauri 620 ambapo kati ya hayo jumla ya mashauri 519 yametolewa maamuzi sawa na asilimia 83.7%.

Kwa upande wa Mahkama za Ardhi za Zanzibar kwa mwaka 2022 zilipokea mashauri mapya mashauri 184 ambapo jumla ya mashauri 204 yakiwemo mashauri ya miaka iliyopita yaliamuliwa na kutolewa maamuzi sawa asilimia 65%,  na kwa hivi sasa Mahkama zote za Ardhi  za Zanzibar zina jumla ya mashauri 193.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Takwimu ziaonesha utendaji kazi wa Mahkama umeboreka na hii inatokana na utaratibu mzuri tuliojiwekea wa Mahakimu na Makadhi kutoa taarifa za utendaji wao kwa siku, wiki na mwezi pamoja na kusimamia nidhamu.

MHESHMIWA MGENI RASMI,

Napenda nieleze kwamba ufanisi katika shughuli zetu za usikilizaji wa mashauri na kuyatolea maamuzi unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa wafanyakazi wa kutosha. Napenda nieleze kwamba hivi sasa katika mhimili wetu wa Mahkama tuna uhaba mkubwa wa wafanyakazi kuanzia Mahakimu na wafanyakazi wengine hali iliyosababishwa na vifo pamoja na kustaafu kazi kwa watumishi mbali mbali. Kwa hivi sasa tuna uhaba wa wafanyakazi 40 ikijumuisha Mahakimu na watumishi wengine.

Hivyo kupitia salamu hizi tunakuomba Mheshimiwa Mgeni Rasmi Mipango ya Kiserikali ikiruhusu basi turuhusiwe kujaza nafasi hizo.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Mahkama imeimarisha mifumo yake ya usimamizi wa nidhamu kwa Maofisa na  watumishi wengine wa Mahkama ambapo kwa sasa imeshatengeneza Kanuni za Maadili (Code of Conduct)  pamoja na kanuni za Malipo ya Mawakili ambapo rasimu za kanuni hizo zimeshawasilishwa katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu  kwa taaratibu za kisheria.

Vile vile kwa upande wa Mahkama ya Kadhi tayari Sheria ya Rasimu ya Sheria mpya ya Mahkama ya Kadhi imeshaiwasilisha Serikalini kwa hatua zaidi. Tunaraji kwamba kupitishwa kwa Sheria hii ya Mahkama ya Kadhi kutaleta mapinduzi makubwa katika utendaji mzima wa kazi wa Mahkama ya Kadhi.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Mbali na hayo, Mahkama imejiwekea mikakati kadhaa katika kufikia lengo lake la kufanya maboresho ya kiutendaji. Mwaka 2022 ulituzindulia Ripoti ya Mahitaji ya Mahkama (Need assessment) ambayo imelezea mapungufu kadhaa ambayo Mahkama inakabiliana nayo. Kwa kutumia ripoti hiyo, kwa mwaka huu tumejipanga kuandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano (5) na Mpango wa Maboresho wa Miaka kumi (10) ambao utakuwa ndio Dira ya kuleta ufanisi katika shughuli zetu .

MHESHMIWA MGENI RASMI,

Kuhusu magizo yako uliyoyatoa kwenye kilele cha Siku ya Sheria mwaka jana 2022 kuhusu  matumizi ya lugha ya kiswahili pamoja na kuanzishwa kwa Mahkama ya Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (Mahkama ya Mafisadi), napenda nieleze kwamba, maagizo hayo tumeyafanyia kazi. Mahkama zimekuwa zikiendelea kutumia Kiswahili kadri iwezekanavyo. Mahakama za Wilaya, Mikoa, kadhi na Mahkama Kuu kwa kiasi kikubwa zinatumia Kiswahili katika kuendesha Mashauri.

Halikadhalika, lugha ya Mahkama ya Mwanzo na Mahkama ya Kadhi ni Kiswahili.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Kuhusu Mahkama ya Rushwa na uhujumu Uchumi tayari tumeshachukuwa hatua za awali za kuwa na Mahkama hiyo. Timu yetu ya wataalamu ilifanya ziara ya kutembelea Mahkama ya namna hiyo kwa wenzetu wa Tanzania Bara na tayari imeshawasilisha Ripoti na hatua zitachukuliwa kwa kushirikiana na Taasisi nyengine za sheria ili kuratibu kuundwa mahkama hiyo hapa Zanzibar. Kwa mnasaba wa suala hilo, Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi yaliyofunguliwa Mahkamani 2022 ni 11, shauri 1 limekamilika na mengine 10 yanaendelea.

Uundwaji wa Mahkama hii itarahisisha usikilizaji wa mashauri ya aina hiyo kwa haraka.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Mikakati ya Mahkama kwa 2023 ni utoaji wa huduma kwa njia ya uwazi, haraka na kuzidisha usimamizi wa nidhamu na uwajibikaji wa wafanyakazi na Mawakili wa kujitegemea na kupunguza Mrundikano wa kesi mahkamani.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Mikakati mengine ambayo tumejiwekea ni kuwa Mahkama rafiki inayofikiwa na wananchi kirahisi na iliyo karibu wananchi pamoja na kusimamia na kuendeleza matumizi ya TEHAMA.

MHESHIMIWA MGENI RASMI,

Kwa kumalizia napenda nitoe shukurani nyingi sana kwako binafsi na Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ujumla kwa mashirikiano makubwa unayotupatia katika kuleta ufanisi wa utendaji kazi kwenye Muhimili wa Mahakama. Katika suala hili napenda kukushukuru sana kwa mambo yafuatayo:-

(a)      Kuimarisha kwa kiasi kikubwa maslahi ya watumishi wa Mahkama.

(b)     Kutupatia kwa haraka muundo wa Utawala wa Mahkama (Judiciary Structure) ambao utatusaidia kuleta ufanisi mkubwa katika kazi zetu.

(c)      Kuongeza idadi ya Majaji 4 na kufikia idadi ya majaji Mahkama kuu ya Zanzibar kuwa kumi na mbili 12;

(d)     Kutupatia Mrajisi wa Mahkama Kuu Mwanamama Shupavu;

(e)      Kuongeza idadi ya Makadhi wanne (4) ambao watasaidia kwa kiasi kikubwa katika kusikiliza mashauri kwa haraka.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Napenda kutoa shukrani maalum na za dhati kwa mahkama ya Tanzania kwa ushirikiano wanaotupatia wa hali mali. Tunaomba mashirikiano haya yaendelee na tuyarasimishe kwa kufikia hatua ya kuwa hati ya makubaliano kwa faida za pande zote mbili.

Vilevile napenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa mlezi na mzee wetu mheshimiwa  Waziri wa Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora Maalim Haroun Ali Suleiman kwa mashirikiano makubwa anayotupatia ikiwemo ushauri, miongozo na mambo ya msingi kabisa katika kufanikisha kazi za mahkama kwani mda wote tunapokuwa na tatizo basi yeye yupo tayari katika kutusaidia. Niseme ahsante sana Mheshimiwa Waziri.

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Vilevile napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Washirika wa Maendeleo kama vile UNDP, UNIDOG, taasisi inayojishughulisha na masuala ya kisheria  Afrika-(JIFA), SACJF, Basel Institute n.k. Bila ya kusahau Taasisi ya Mwamvuli wa Mtandao wa Haki za Binadamu (THRDC)

MHESHIMIWA MGENI RASMI;

Shukrani zangu nyengine za dhati ziwaendee Majaji wa Mahkama Kuu, Warajisi watendaji wengine wa Mahkama ambao tumefanyakazi kwa pamoja kwa mwaka huu wa Mahakama.

Mwisho napenda kuwashukuru wale wote waliochangia katika kufanikisha sherehe zetu za mwaka huu wakiwemo wafadhili wetu katika sherehe za Law Day Marathon hususan ikiwemo Kamati iliyoandaa na Kusimamia Matembezi ikiongozwa na mwenyekiti wake Bw. Bagash wa Rahisi Solution. Hatuna cha kuwalipa zaidi ya kuwaambia ahasanteni sana.

MHESHMIWA MGENI RASMI,

Baada ya kusema hayo, sasa kwa heshima na taadhima nakuomba ufanye mambo yafuatayo:-

(i)        Utuzindulie bendera ya Mahkama pamoja  nembo ya Mahkama.

(ii)      Upokee ripoti ya utendaji kazi wa Mahkama kwa mwaka 2022.

(iii)    Upokee zawadi maalum ya Mahkama ilyoandaliwa kwa ajili yako.

MHESHMIWA MGENI RASMI,

Baada ya mambo hayo nitakuomba kwa heshima na taadhima uihutubie hadhara hii ambayo ina hamu kubwa ya kusikiliza nasaha na maelekezo yako.


‘’MHESHIMIWA MGENI RASMI KARIBU SANA’’


Unguja

High Court, Vuga
ZANZIBAR
Tel: +255 719 606 436
Email: info@judiciaryzanzibar.go.tz
Monday - Friday: 07:30am - 09:30pm
Saturday & Sunday: Closed

Pemba

High Court, Chake-Chake
ZANZIBAR
Tel: +255 719 606 436
Email: infopemba@judiciaryzanzibar.go.tz
Monday - Friday: 07:30am - 09:30pm
Saturday & Sunday: Closed