HUTUBA YA WAZIRI LUKUVI KATIKA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI MAHKAMA YA WILAYA YA MKOA
HOTUBA YA MHE. WILLIAM V. LUKUVI (MB.) WAZIRI WA
NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU) KATIKA HAFLA YA UWEKAJI WA
JIWE LA MSINGI KATIKA UJENZI WA JENGO JIPYA LA MAHKAMA YA WILAYA YA MICHEWENI
TAREHE 04 JANUARI, 2025
Mheshimiwa Khamis Ramadhani Abdalla, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Rashid Hadidi Rashid, Mkuu wa Mikoa wa Kusini
Pemba;
Ndugu Yusuph Ali Juma, Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa Kusini Pemba;
Waheshimiwa Majaji mliopo mkiongozwa na Mhe.
Jaji Salum Hassan Bakar, Jaji Mkazi - Pemba;
Mheshimiwa Othman Ame Chumu, Naibu Kadhi Mkuu;
Mheshimiwa Hamad Omar Bakar, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani;
Waheshimiwa Wabunge na Wawakilishi mliopo;
Mheshimiwa Valentina Katema, Mrajis wa Mahkama Kuu;
Waheshimiwa Mahakimu na Makadhi wa ngazi mbali
mbali;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na
Serikali;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama wa SMT na
SMZ mliopo;
Waheshimiwa Mawakili wa Serikali na Mawakili wa
Kujitegemea;
Ndugu Watumishi wa Umma na Wanahabari mliopo;
Wageni Waalikwa - Mabibi na Mabwana.
Assalaam Aleiykum
Mheshimiwa Jaji Mkuu, Ndugu Viongozi mliopo na
wananchi wote.
Niungane na
walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwingi wa rehma kwa
kutujaalia uzima na afya iliyotuwezesha kukutana katika hafla hii muhimu ya
uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya
Micheweni.
Pili niwaashukuru
sana kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hii adhimu. Mwaliko wenu
umenipa fursa ya kujumuika na Wananchi wenzangu hususani wa Wilaya ya Mkoani pamoja
na wananchi wengine waliofika katika sherehe hii ya uwekaji wa jiwe la msingi
la ujenzi wa jengo jipya la Mahkama ya Wilaya ya Mkoani hapa Changaweni. Sambamba
na hilo, niwashukuru na kuwapongeza viongozi na wananchi wote mliojitokeza
katika sherehe hii ambayo ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Ndugu Viongozi na wananchi wote,
Sote ni mshahidi
wa hatua kubwa za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kupitia uongozi wa awamu ya nane chini ya Mhe. Daktari Hussein Ali
Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Mafanikio ya
Serikali ya awamu ya nane yanaonekana wazi katika nyanja za siasa na utawala
bora, uchumi, huduma za kijamii na namna utamaduni wa watu wa Visiwa vya
Zanzibar unavyoenziwa na kuheshimika wakati wote.
Maendeleo katika
nyanja hizi yanashuhudiwa vizuri katika maeneo mbalimbali kupitia ujenzi wa
miundombinu ya mawasiliano, majengo ya ofisi, majengo ya kutolea huduma za
kijamii pamoja na msisitizo uliowekwa kwenye uchumi wa buluu, uvuvi na kilimo
cha mwani. Kwa upande wa ujenzi wa majengo
ya Ofisi, mpango ya Serikali ya Zanzibar ni kuhakikisha yanajengwa majengo ya
kisasa ya ofisi ili kuimarisha mazingira bora ya kufanyia kazi na kuchochea
utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ndugu Viongozi na wananchi wote,
Tunafahamu kwa
miaka mingi Mahakama zetu zimekuwa na changamoto za miundombinu ya majengo. Kwa
mfano jengo linalotumika hivi sasa kwa shughuli za Mahakama ya Wilaya halikidhi
mahitaji halisi ya Mahakama kwa sasa. Pamoja na ufinyu wa nafasi, jengo hilo
pia si rafiki kwa watumiaji wenye mahitaji maalumu. Wananchi wanaofika kufuata
huduma muda mwingi wanakosa sehemu maalum ya kupumzikia au kusubiri kuhudumiwa.
Hali hii ndiyo iliyoipelekea
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuchukua hatua za makusudi kuja na mradi wa
ujenzi wa jengo hili la Mahakam ya Wilaya pamoja na majengo mengine ya Mahakama
za Mikoa na Wilaya kule Unguja na hapa Pemba. Hivyo, ujenzi wa jengo hili ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa
majengo saba ambao ulipangwa kufanyika katika mwaka wa fedha wa 2023/2024. Kwa
upande wa Pemba, mradi huu wa Loti Nambari 2 unajumuisha majengo matatu
(Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini, Mahakama ya Wilaya ya Michweweni na Mahakama ya
Wilaya ya Mkoani hapa Changaweni)
Ndugu Viongozi na wananchi wote,
Kwa upande wa
jengo hili, ujenzi wake ukamilika utatatua changamoto ya mahitaji ya ofisi kwa
watumishi wa Mahakama na wadau wake wakiwemo Mawakili wa Serikali na wa
Kujitegemea, Jeshi la Polisi, Chuo cha Mafunzo, Ustawi wa Jamii, Msaada wa
Kisheria, wananchi kwa ujumla na mahabusu wanao fika kusikiliza mashauri.
Aidha, nimeonyeshwa namna jengo hili lilivyosanifiwa kukidhi mahitaji ya sasa
na ya wakati ujao na kwamba limezingatia pia mifumo yote ya kiusalama na
matumizi ya Teknologia ya Habari na Mawasiliano.
Ndugu Viongozi na wananchi wote,
Serikali
inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya majengo ya
ofisi, hivyo ni wajibu wa watumiaji wa miundombinu hii na wananchi kwa ujumla
kuitunza ili iweze kudumu kwa miaka mingi ijayo. Kudumu kwa majengo haya
kunahitaji matunzo endelevu, usafi na matumizi sahihi ya umeme na mashine
zilizomo ndani au mifumo ya huduma mbali mbali ndani ya majengo. Hivyo, ni
muhimu uongozi wa Mahakama kuandaa mkakati maalum wa matunzo ya majengo yake
yote yanayojengwa ili uimara na haiba yake vibakie kwa miaka mingi ijayo pasina
kutetereka.
Ndugu viongozi na ndugu wananchi
Nihitimishe hotuba
yangu kwa kukushukuru kwa dhati Mheshimiwa Jaji Mkuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Zanzibar pamoja na wote walioshiriki katika maandalizi ya hafla hii inayoakisi
maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964. Kwa dhati kabisa niishukuru
na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Mhe. Daktari
Hussein Ali Mwinyi kwa hatua zake za kuujengea uwezo Muhimili huu wa Mahakama
ili uweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na uhuru zaidi.
Niwashukuru pia
viongozi na wananchi wote mliofika na kujumuika katika sherehe hii. Bila shaka,
uwepo wenu hapa una maana kubwa katika kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
ambayo tarehe 12 Januari, 2025 yatatimiza miaka 61. Kipekee nimpongeze Mshauri
Mwelekezi anaesimamia ujenzi huu Kampuni
ya EDGE Consult pamoja na Mkandarasi Kampuni
ya Ujenzi ya JKU kwa kazi wanazoendelea kuzifanya. Niwahimize kukamilisha
ujenzi huu kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa ili jengo hili lianze kutumika kama
ilivyopangwa.
Mwisho lakini si
kwa umuhimu, niwashukuru na kuwapongeza wenzetu wa Muhimili huu wa Mahakama
hususani Waheshimiwa Majaji na Waheshimiwa Mahakimu kwa kuendelea kutekeleza
wajibu wenu wa kutafsiri sheria na kusimamia utoaji wa haki nchini. Niwaombe na
kuwasihi kuendelea kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi, weredi na uadilifu
mkubwa. Niwasihi pia wadau wote kuendelea kuuheshimu Muhimili huu na kulinda
uhuru wake ili wasikutane na vikwazo wakati wa utekelezaji wa majukumu hayo
muhimu. Serikali kwa upande wetu tutaendelea kujenga miundombinu wezeshi ikiwemo
majengo kama haya ili kuwawezesha kufanya kazi katika mazingira mazuri
kiutendaji.
Asanteni sana kwa kunisikiliza
__________