Registrar: registrar@judiciaryzanzibar.go.tz | Chief Court Administrator: cca@judiciaryzanzibar.go.tz

THE JUDICIARY OF ZANZIBAR

JAJI MKUU AWAAFISHA MAKADHI WA MIKOA

HOTUBA YA MHE. JAJI MKUU WA ZANZIBAR KWENYE HAFLA

YA KUAPISHWA MAKADHI WAPYA WA MIKOA.

PAHALA: MAHKAMA KUU TUNGUU

TAREHE: 17/12/2024

Wahe. Majaji wa Mahkama Kuu mliopo,

Mhe. Mwenyekiti, Tume ya Utumishi ya Mahkama na Wajumbe wako wote,

Mhe. Kadhi Mkuu,

Mhe. Naibu Kadhi Mkuu,

Wahe. Kadhi wa Rufaa mliopo,

Mhe. Mrajis wa Mahkama Kuu

Mtendaji Mkuu wa Mahkama,

Mhe. Kaimu mrajis wa Mahkama ya Kadhi,

 Rais wa Chama Cha Mawakili

Wahe. Naibu Warajis wa Mahkama Kuu mliopo,

Muwakilishi kutoka Wizara ya Nchi Afisi ya Rais,

Katiba, Utumishi na Utawala Bora,

Muwakilishi kutoka Afisi ya Mufti Mkuu,

Muwakilishi kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana,

Wakurugenzi wote wa Mahkama mliopo,

Wahe. Mahakimu na Makadhi mliopo,

Mawakili wa Serikali na Binafsi mliopo,

Wafanyakazi wote wa Mahkama,

Wanahabari,

Waalikwa wote,

Mabibi na mabwana,

ASALAMU ALAIKUM:

Kwanza kabisa, hatuna budi kumshukuru M/Mungu mwingi wa rehma na utukufu kwa kuturuzuku neema ya uhai na afya njema na kutuwezesha kuhudhuria hapa kushuhudia tukio hili adhimu la kihistoria la kuapishwa kwa Waheshmiwa Makadhi watano (5) wa Mkoa kwa Mikoa ya Unguja na Pemba baada ya kuteuliwa na Tume ya Utumishi ya Mahkama.

Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuruni nyote mliohudhuria kwa kuacha majukumu yenu muhimu na kukubali kuhudhuria kwenye shughuli yetu hii. Sambamba na hayo na kwa kiupekee, nachukua fursa hii kuwapongeza sana Makadhi walioapishwa leo ambao ni (1) Mhe. Omar Sheha Khamis (2) Mhe. Abdulrahman Omar Bakar (3) Mhe. Masoud Said Abdalla (4) Mhe. Abdul – Aziz Saleh Juma na, (5) Mhe. Abdalla Hamad Salum kwa kuteuliwa kuwa Makadhi wa Mkoa.  Kwa niaba ya Mahkama Kuu ya Zanzibar, ninawatakia kila la kheri na mafanikio katika kutekeleza majukumu yenu mapya.

Vilevile, natoa wito kwa wale wote ambao waliomba nafasi hizi na hawakubahatika, kwamba, wawe wastahmilivu na waendelee kuchapa kazi huku wakielewa kuwa, hali hiyo, haimainishi kwamba, hawana uwezo bali ni kutokana na uchache tu wa nafasi, na kwa kweli bado zipo fursa nyingi tu  zilizo mbele yao.

Wahe. Makadhi na waalikwa wote;

Napenda ieleweke kuwa, uteuzi huu wa  Makadhi wa Mahkama za Kadhi za  Mkoa, umekuja kufuatia uamuzi wa Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kutunga  Sheria Mpya ya Mahkama za Kadhi Nam. 8 ya 2023 ambayo pamoja na mambo mengine, imeanzisha nafasi ya Kadhi wa Mahkama ya Kadhi ya Mkoa, kwa lengo la kutanuwa wigo zaidi katika upatikanaji wa haki kwa mashauri ya  Mahkama za Kadhi. Kwa mnasaba huo, nachukua fursa hii kuipongeza sana Serikali yetu na pia, naipongeza sana Tume ya Utumishi ya Mahkama kwa kusimamia vizuri na kwa uadilifu mkubwa mchakato wote wa usaili wa waombaji  walioomba nafasi hizi za Makadhi wa Mkoa hadi hatua hii ambapo leo tunafurahia kupata Makadhi wa mikoa. Kwa kweli, nikiwa mkuu wa mhimili huu wa Mahkama, nimeridhishwa na namna zoezi hilo lilivyofanyika kwa haki, bila ya upendeleo wala ushawishi wa aina yoyote.

Wahe. Makadhi na waalikwa wote;

Nitakuwa mchoyo wa fadhila, kama sitatowa shukrani zangu binafsi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Mwalimu Haroun Ali Suleiman pamoja na  Wizara yetu ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kwa ujumla, kwa mashirikiano yake makubwa  kwa mhimili wetu wa Mahkama hususan kwa kutupatia kibali cha kuajiri makadhi hawa watano (5) pamoja na watumishi mbali mbali wa Mahkama.

Wahe. Makadhi na waalikwa wote;

Mahkama ya Kadhi si chombo kipya katika utaratibu wa kimahkama Zanzibar, bali ni Mahkama kongwe ambayo awali ilianzishwa katika utawala wa Sultani katika mfumo usiokuwa rasmi kisheria mwaka 1832, ambapo kabla ya hapo jamii ilikuwa ikitatua migogoro yake kwa kupitia Mashekhe ndani ya jamii husika.

Katika kipindi cha Himaya ya Muingereza mbali na kuanzishwa kwa mfumo wa Mahkama nyengine mwaka 1897, Mahkama ya Kadhi pia iliimarishwa zaidi na kuwekewa taratibu zake maalumu kisheria. Mahkama ya Kadhi ilipita katika vipindi tofauti katika utendaji wake wa kazi za utoaji wa haki na usimamizi wa sheria, ambapo Mahkama hii kabla na baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya 1964, iliongozwa na Dikrii mbalimbali za Mahkama ikiwemo Dikrii ya mwaka 1966 ambayo ilifanya mabadiliko madogo tu.

Mnamo mwaka 1985, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha rasmi Mahkama za Kadhi chini ya Mahkama Kuu ya Zanzibar kwa Sheria Nam. 3 ya 1985, ambayo pia ilifanyiwa marekebisho madogo na Sheria Nam. 4 ya 2003. Kuanzishwa kwa Mahkama za Kadhi kumetokana na msingi wa kikatiba kwa mujibu wa kifungu cha 100 cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 kinacholipa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar mamlaka ya kuanzisha Mahkama nyenginezo chini ya Mahkama Kuu. Vilevile tukirudi katika kifungu cha 5 cha Sheria ya Mahkama Kuu Nam. 2 ya 1985 kimebainisha mahkama zilizochini ya Mahkama Kuu ambapo miongoni mwazo ni Mahkama za Kadhi.

Katika kuzipa nguvu zaidi Mahkama za Kadhi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2017 ilifanya marekebisho makubwa kwa kufuta Sheria Namba 3 ya 1985 na kupatikana sheria mpya, Sheria Namba 9 ya 2017, ambapo sheria hiyo vilevile ilikuja kufutwa hivi karibuni na Sheria mpya ya Mahkama za Kadhi Nam. 8 ya 2023 kwa lengo la kuendana na wakati, kuongeza ufanisi pamoja na kutanua wigo katika upatikanaji wa haki, ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa ngazi ya Mkoa ambayo leo hii kwa mara ya kwanza tumeanza utekelezaji wake kwa kuwateuwa Makadhi wa Mkoa, kwani ngazi hii haikuwepo katika katika muundo wa Mahkama za Kadhi katika sheria zote zilizotangulia kuanzisha Mahkama za Kadhi Zanzibar.

Wahe. Makadhi na waalikwa wote;

Jukumu la kuhukumu na kufanya haki baina ya waliohasimiana ni kubwa na zito mno. Hivyo, kupitia hafla hii, napenda nitowe wito kwa Waheshmiwa Makadhi wa Mkoa ambao mmekula viapo hivi punde, kuzitumikia nafasi mlizopewa kwa kutenda haki na kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kwa ubunifu wa hali ya juu huku mkijuwa kuwa, nafasi mlizozipata ni amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ambapo atatuuliza siku ya kiama namna tulivyozitumikia nafasi zetu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuasa katika Qur-an sura ya 4 aya ya 58 kama alivyosema; na hapa ninanukuu tafisiri yake:

"Na mnapohukumu baina ya watu muhukumu kwa uadilifu"

 Pia tuikumbuke, bali iwe ndio dira yetu kauli ya Mtume juu yake rehma na amani pale aliposema; na hapa ninanukuu tafsiri yake:

"Mwenye kutawalishwa jukumu la kutoa maamuzi ya kimahkama, bila shaka amechinjwa bila ya kutumia kisu"

Hapa napenda ieleweke kwamba, licha ya kuwa aya na hadithi nilizonukuu zimejikita zaidi katika kusisitiza uadilifu, lakini pia tuna wajibu wa kutambua kuwa kufanya shughuli za kimahkama kwa uadilifu na haki kuna malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, hili linathibitishwa na Swahaba Abdallah Bin Masoud pale aliposema; na hapa ninanukuu tafsiri yake:

“Wallahi, kufanya kazi ya kutoa hukumu (kwa haki) siku moja tu, basi kwangu ni bora kuliko ibada ya miaka sabiini”

Wahe. Makadhi na waalikwa wote;

Jukumu kuu la Mahkama ni kutoa haki ambapo kimsingi jukumu hili ni la kiungu, hivyo tuna wajibu wa kufahamu kwamba Mwenyezi Mungu anakuwa pamoja na Kadhi, Hakimu au Jaji pale tu atakapotenda haki na kufanya uadilifu, ama pale anapoanza kuikaribisha dhulma na kwenda kinyume na maadili ya kazi yake, Mwenyezi Mungu hujitenga naye na huanza kutawaliwa na shetani.

Kwa muktadha huo, kupitia shughuli hii, ninatowa wito kwenu makadhi wapya na wakongwe kwamba, mfanye kazi kwa kujiamini na kufuata sheria na msikubali kuingiliwa na mtu ama taasisi yoyote katika kutekeleza majukumu yenu. Aidha, napenda muelewe kuwa, nyinyi ni vioo vya jamii na kwa hivyo, mnapaswa kufanya kazi zenu kwa kuzingatia maadili ya viongozi wa umma pamoja na kujiepusha na rushwa za aina zote.

Sambamba na hayo, ninawakumbusha waheshmiwa Makadhi na viongozi wote wa Mahkama kuwa, kujaza Fomu za Tamko la Viongozi wa Umma kuhusu raslimali na madeni, ni miongoni mwa maadili na kutokujaza fomu hizo ni kuvunja maadili. Hivyo, sote tujazeni fomu hizo kabla ya muda kumalizika tarehe 31/12/2024.

Wahe. Makadhi na Waalikwa wote;

Sote tunaelewa kuwa jukumu la msingi la Mahkama ni kupokea, kusikiliza na kutolea maamuzi mashauri yote ya jinai na madai, sambamba na kutenda haki kwa wananchi wote bila ya chuki, woga ama upendeleo vilevile kuhakikisha kuwa maamuzi yanatolewa kwa uweledi na haraka.

Katika kuhakikisha hili linatendeka sambamba na kulinda maadili, Mahkama imetayarisha Kanuni za Maadili (Code of Conduct) zinazowagusa watumishi wote wa Mahkama, pia tumeanzisha Kamati ya Maadili ya Mahakimu, Makadhi na Watumishi wengine wa Mahkama inayoongozwa na Jaji wa Mahkama Kuu, vilevile kuna kitengo cha usimamizi wa maadili ambacho kinaongozwa na Naibu Mrajis wa Mahkama Kuu. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa watumishi wa Mahkama wanafanya kazi zao kwa misingi ya maadili ya hali ya juu ili kuongeza na kukuza  imani ya wananchi na Serikali kwa mhimili wa Mahkama.

Wahe. Makadhi na Waalikwa wote;

Napenda niwaeleze kuwa, Mahkama za Kadhi zina umuhimu mkubwa kwa maisha ya wazanzibari ambao kwa asilimia kubwa ni waislamu. Kwa sababu hiyo, asilimia kubwa ya mashauri ya kijamii yanayowahusu waislamu kama vile ndoa, talaka, mgawanyo wa mali iliyopatikana kwenye ndoa baina ya wanandoa, mirathi, wasia, hiba, wakfu, matunzo na malezi ya watoto na kadhalika husikilizwa kwenye Mahkama hizi.

Kwa kuona umuhimu huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imechukuwa hatua kubwa  za kuandaa mazingira mazuri ya utendaji kazi na utoaji haki kwa Mahakama za Kadhi pamoja na Mahkama za kawaida kwa ujumla.

Miongoni mwa hatua hizo ni ujenzi unaoendelea wa majengo ya kisasa ya Mahkama Unguja na Pemba ambapo majengo yote hayo yana ofisi za kutosha pia kwa Mahkama zetu za Kadhi. Vilevile kutangazwa kwa Sheria mpya ya Mahkama za Kadhi Nam. 8 ya 2023 pamoja na kanuni za uendeshaji wa mashauri katika Mahkama hizo ni miongoni mwa mambo yatakayoziwezesha Mahkama za Kadhi Zanzibar kufanya kazi zake kwa uweledi mkubwa zaidi kama zilivyo mahkama za kawaida sambamba na kuzipa mamlaka pale inapobidi, Mahkama za Kadhi kutoa adhabu kwa wale wote watakaopatikana na hatia ya kudharau na kukaidi amri za Mahakama.

Wahe. Makadhi na Waalikwa wote;

Katika kipindi hichi tumeshuhudia maboresho makubwa kwa upande wa Mahkama za Kadhi na Mahkama za kawaida kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na ongezeko la Makadhi kwa upande wa Mahkama zetu za Kadhi na watumishi wengine wa Mahkama, maslahi bora kwa watumishi wote wa Mahkama, mafunzo mbali mbali ya kuwajengea uwezo makadhi na watumishi wengine wa Mahkama sambamba na kupatiwa vifaa vya kutendea kazi kama vile Kompyuta aina ya laptops na vishkwambi.

Vilevile kumekuwa na ongezeko la fedha za kuendeshea ofisi (O.C) kwa shughuli za Mahkama ya Kadhi, hivyo kutoa fursa kwa Mahkama hizi kuweza kuendesha baadhi ya mambo yake muhimu bila ya kugongana na Mahkama Kuu, kama ambavyo kumekuwa na ushirikishwaji mkubwa wa makadhi katika shughuli zote za kimahkama.

Kwa kweli, hatuwa zote hizo zilizochukuliwa na Serikali na Uongozi wa Mahkama, zimeifanya Mahkama za Kadhi kuwa ni za kisasa zaidi na zinayokwenda na wakati na kuondokana na hali iliyokuwepo zamani ambapo Mahakama za Kadhi zilionekana kama uchochoro mdogo ndani ya mhimili wa Mahkama na hata kupelekea baadhi ya watu kuzidharau. Hivyo, kutokana na hatua hizo za Serikali, hivi sasa hadhi ya Mahkama zetu za Kadhi kitaifa na kimataifa imekuwa, na nina kila sababu ya kusema kuwa, hayo ni mafanikio makubwa kwetu ambapo tunapaswa kujipongeza.

Wahe. Makadhi na Waalikwa wote;

Napenda kuchukuwa fursa hii kuwapongeza Makadhi wote kwa utendaji kazi wenu mzuri na wa kizalendo. Kwa kweli malalamiko dhidi ya Mahkama za Kadhi yamekuwa ni machache mno. Hukumu zinazotolewa sio tu kuwa zinakidhi viwango vya kisheria lakini pia ni hukumu zilizofanyiwa tafiti za kina (well reserched judgments) ambapo wasomi mbali mbali na wanafunzi wanaweza kuzitumia katika tafiti zao. Aidha, wadaawa hupatiwa mienendo ya mashauri kwa haraka, kwa hivyo hongereni sana.

Kitu ninachotaka kusisitiza kwa Makadhi wapya na hata wale wa zamani ni kwamba, tusiridhike na viwango vyetu vya elimu tulivyonavyo bali tujiongeze kwa kujifunza zaidi katika nyanja tofauti ili tusiachwe nyuma na mabadiliko ya sayansi na teknologia yanayotokea ulimwenguni.

Kwa mfano, hivi sasa miamala mingi inayohusu migogoro ya Mahkama za Kadhi kama vile ndoa, talaka na mizozo mbali mbali huhusisha tehama, na kwa hivyo hatuna budi kujifunza zaidi fani hii ya teknologia ya habari na mawasiliano ili tufanye kazi zetu kwa ufanisi wa hali ya juu kama vile mshairi mmoja wa kiarabu alivyosema, na hapa nanukuu tafsiri yake:

“Kuwa mwenye kupata faida kila siku kwa kuongeza elimu na ogelea kwenye bahari ya faida”

Wahe. Makadhi na Waalikwa wote,

Mashirikianao na wadau (stakeholders cooperation) ni moja kati ya eneo muhimu katika utendaji wa kazi zetu. Mahkama haitaweza kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa peke yake, ni lazima tukuze mashirikiano na wadau wetu mbali mbali. Kwa mnasaba huu, hivi karibuni, kwa makusudi tumechukua hatua ya kuanzisha Kamati ya Kusukuma Mbele Mashauri ya Mahkama za Kadhi ambayo, wajumbe wake ni maofisa kutoka Mahkama ya Kadhi na wadau wengine mbalimbali, kama vile Chama cha Mawakili, Afisi ya Mufti Mkuu, Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, nakadhalika.

Hivyo, naendelea kusisitiza kufanyika kwa vikao vya kamati hiyo kwa kila robo mwaka. Uzoefu unaonyesha kuwa, kamati hizi husaidia sana katika kusukuma usikilizaji wa mashauri kwa haraka pamoja na kuondoa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa shughuli zetu na kupunguza misuguano au kuonesheana vidole baina ya Taasisi zetu za haki.

Wahe. Makadhi na Waalikwa wote,

Kwa kumalizia, napenda nitowe wito kwa watumishi wote wa Mahkama kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazowea bali tuhakikishe tunafanya kazi kwa kuzingatia sheria tukiongozwa na uadilifu, uweledi pamoja na uwajibikaji wa hali ya juu.

Mwisho kabisa, nawatakieni nyote kila la kheri na mafanikio katika kutekeleza majukumu yenu.

 


Unguja

High Court, Vuga
ZANZIBAR
Tel: +255 719 606 436
Email: info@judiciaryzanzibar.go.tz
Monday - Friday: 07:30am - 09:30pm
Saturday & Sunday: Closed

Pemba

High Court, Chake-Chake
ZANZIBAR
Tel: +255 719 606 436
Email: infopemba@judiciaryzanzibar.go.tz
Monday - Friday: 07:30am - 09:30pm
Saturday & Sunday: Closed