JAJI MKUU AFUNGA KIKAO KAZI BAINA YA MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI (WCF) NA WATENDAJI WA MAHKAMA
Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla
amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa mstari wa mbele katika kuziimarisha
na kuzijengea uwezo Mahakama pamoja na
vyombo vyote vya utatuzi wa migogoro ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwa na sheria
rafiki za kazi zinazoakisi mazingira halisi ya Tanzania.
Ameyasema hayo wakati wa kufunga kikao kazi baina
na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na
Viongozi wa Mahkama ya Tanzania
Aidha amewataka watendaji wa Mahakama na wadau
wote wa taasisi za Kazi kutumia umahiri na uweledi wao katika kuhakikisha kuwa
wafanyakazi wanapata stahiki zao kwa haraka ikiwa ni pamoja na
kupata fidia kutokana na majanga mbali
mbali yanayowapata kama vile vifo,
maradhi, ulemavu wakiwa katika kutekeleza majukumu yao ya kazi
Vile vile Mhe Khamis
alisema Ni lazima tuwe na mifumo
inayosomana kwa lengo la kuondoa urasimu na pingamizi zote zinazochelewesha kulipwa fidia kwa wafanyakazi.
“Ni
lazima tuendelee kuwajengea uwezo watumishi wetu wa taasisi za kazi ili waweze
kutoa huduma bora kwa wafanyakazi na wananchi kwa ujumla”, amesema.
Mhe Jaji Khamis
ametoa wito kwa ZSSF kuongeza juhudi zaidi ya kukuza uelewa wa
mambo ya fidia kwa wafanyakazi na mafao mbali mbali yanaotolewa na ZSSF kwa
wafanyakazi na wadau mbali mbali, kwa
vile hivi sasa masuala ya fidia kwa wafanyakazi yanashughulikiwa na ZSSF kutokana na
mabadiliko ya Sheria Nam. 15/86.
Sambamba na hayo Jaji Khamis aliipongeza Mifuko ya Fidia kwa wafanyakazi Tanzania yaani WCF na
ZSSF kwa mashirikiano yao na jitihada zao kubwa wanazochukua katika kuwajengea
uwezo maafisa wa Mahkama juu ya sheria na mambo mbali mbali ya kikazi. akitolea
mfano, kwa mwaka huu wa 2024, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF)
uliendesha mafunzo kwa Mahakimu juu ya taratibu na mambo msingi ya kuzingatia
katika uendeshaji wa mashauri ya jinai na madai yanayohusu ZSSF.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma,
akizungumza katika hafla hiyo, amesema kufanyika kwa Kikao Kazi Zanzibar ni kutanua
uwigo wa kuhakikisha kwamba ujuzi walionao Tanzania Bara ni huo huo walionao Zanzibar
ili kuleta ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi wanaowahudumia.
Nae kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Kazi Jaji Dkt. Yose Mlyambina aliiushukuru uongozi
wa Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi Tanzania
kwa kuwezesha kufanya kikao kazi hicho.
Kikao kazi hicho kiliwashilikisha Majaji wa
Mahkama Kuu ya Tanzania, Majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar na watendaji kutoka
vitengo cha kazi vya Tanzania bara na Zanzibar